Habari

Imewekwa: Oct, 28 2025

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHENGE” KATIKA ENEO KUSINI MASHARIKI MWA BAHARI YA HINDI

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHENGE” KATIKA ENEO KUSINI MASHARIKI MWA BAHARI YA HINDI

Dar es Salaam, 27 Oktoba, 2025 Usiku:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kilichokuwa Kimbunga “CHENGE” katika katika maeneo ya pwani ya nchi yetu.

Kimbunga “CHENGE” kimepoteza nguvu yake na kusambaratika kabisa wakati kikikaribia ukanda wa pwani ya nchi yetu. Hata hivyo, mvua na mawingu yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yamesambaa katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan katika mikoa ya Lindi, Pwani, Dar es salaam na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba na kusababisha vipindi vya mvua katika baadhi ya maeneo hayo. Kwa mfano hadi kufika saa 12 jioni ya leo, kituo cha hali ya hewa kilichopo uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Dar es salaam kimeripoti mvua ya milimita 9.1 kwa kipindi cha saa 9 zilizopita. Vilevile katika kipindi hicho, kituo cha hali ya hewa kilichopo katika bandari ya Dar es Salaam kimeripoti mvua ya milimita 3.5.

Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa mabaki ya Kimbunga hicho yanatarajiwa kuendelea kusababisha vipindi vichache vya mvua kwa usiku wa leo tarehe 27 na siku ya kesho 28 ya Mwezi Oktoba, 2025 kwa maeneo ya mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo jirani. Hata hivyo, hakuna madhara makubwa yanayotarajiwa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mabaki ya kimbunga “CHENGE” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

USHAURI: Watumiaji wa Bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.