Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

ISO 9001:2015 Imethibitishwa Kutoa Huduma za Hali ya Hewa kwenye Usafiri wa Anga

TMA YABAINISHA NJIA RASMI ZINAZOTUMIKA KATIKA USAMBAZAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

News Image

Zanzibar,  Tarehe  12/01/2026

TMA imebainisha njia rasmi zinazotumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa nchini, hayo yalizungumzwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ofisi ya Zanzibar, Ndg. Masoud Makame Faki alipokuwa anazungumza na wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kuwakaribisha kutembelea banda la TMA lililopo kwenye Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (ZITF) yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nyamanzi kuanzia Tar 29 Disemba 2025 hadi 16 Januari, 2026.

" Ninawasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa kupitia njia rasmi zinazotumika na TMA ikiwemo vyombo vya habari vilivyorasimika, Blogs na Tovuti ya Mamlaka (www.meteo.go.tz), pamoja na mitandao ya kijamii ya Mamlaka ikihusisha, YouTube channel, instagram, tweeter, what's app channel na facebook ambazo akaunti zake unaweza kuzipata moja kwa moja kwenye kurasa ya mwanzoni mwa tovuti ya Mamlaka." Alisisitiza Ndugu Faki

Aidha, ndugu Faki aliongezea kusema kuwa wananchi wanapaswa kuachana na tabia za usambazaji wa taarifa potofu wanazozikuta mitandaoni sababu zinaweza kuathiri mipango ya kimaendeleo inayoratibiwa nchini, na badala yake wafuatilie taarifa za hali ya hewa kupitia njia rasmi zilizobainishwa na Mamlaka.

Kupitia maonesho hayo, TMA imeendelea kutoa elimu na ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali ya hali ya hewa ikiwemo suala la fukuto la joto linaloendelea visiwani hapo, akisema kwa sasa wakati Dunia inaendelea na mzunguko wake kuelekea katika kizio cha kusini kunakuwa na jua la utosi inapelekea hali ya joto kuongezeka, hivyo kutokana na kisiwa hicho kuzungukwa na maji imepelekea unyevu kuwa mwingi angani na kufanya wakazi kukumbwa na fukuto la joto linaloendelea.