Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

ISO 9001:2015 Certified in Aviation Meteorological Services

Habari

 • KIMBUNGA KENNETH

  Imewekwa: 26th April, 2019

  Taarifa hii inatoa mrejeo wa mwenendo wa kimbunga “Kenneth” katika bahari ya Hindi na athari zake kwa maeneo mbalimbali hapa nchini.

  Katika kipindi cha siku mbili zilizopita (24 na 25 April 2019), kimbunga (Kenneth) kiliendelea kuimarika na nguvu ya mgandamizo katika kitovu chake (Central Pressure) ilifikia kipimo cha 934 hPa. Nguvu ya kimbunga ilipungua kulipoingia nchi kavu mchana wa tarehe 25 Aprili 2019 kama ilivyokuwa imetabiriwa. Ilipofika saa 9 usiku wa kuamkia tarehe 26 Aprili 2019 kimbunga kilifika nchi kavu kaskazini mashariki mwa Msumbiji (12.4S/39.6E) takribani kilometa 220 kusini mwa Mtwara, hivyo nguvu ya kimbunga ilipungua zaidi na mgandamizo katika kitovu (Central Pressure) kufikia kipimo cha 995 hPa na nguvu ya upepo kufikia kasi ya kilometa 70 kwa saa, hivyo kupelekea kubadilika kutoka kimbunga kamili na kuwa mgandamizo mdogo (Overland Depression “EX-KENNETH”). Taarifa za uangazi katika kufuatilia madhara ya mwenendo wa kimbunga hicho “Kenneth”, kama zilivyo pimwa katika kituo cha hali ya hewa kilichopo Mtwara, zinaonesha upepo wa kasi ya kilometa 60 kwa saa na mvua ya milimita 10.1. Anga la Mtwara lilikuwa limefunikwa na mawingu mazito kwa siku zote mbili.

  Matarajio ni kwamba mgandamizo mdogo (Overland Depression) “EXKenneth” utaendelea kupungua nguvu huku kikisogea kuelekea kusini-mashariki mwa msumbiji ifikapo mchana wa tarehe 27 Aprili 2019. Mchana wa leo tarehe 26 Aprili 2019, mgandamizo huo mdogo unatarajiwa kuwa umbali wa takribani kilomita 297 kusini mwa Mtwara.

  Jedwali lifuatalo linaelezea utabiri wa mwenendo wa mgandamizo huo mdogo (EX-Kenneth) kwa siku mbili zijazo.

  Muda

  Eneo kilipo

  Umbali kutoka pwani ya Mtwara

  Kasi ya juu ya upepo

  26/04/2019 Mchana

  12.70S/39.20E

  (Juu ya ardhi ya Msumbiji)

  Km 297

  Km 70 kwa saa

  26/04/2019 Usiku

  13.00S/39.50E

  (Juu ya ardhi ya Msumbiji)

  Km 330

  Km 50 kwa saa

  27/04/2019 Asubuhi

  12.70S/39.70E

  (Juu ya ardhi ya Msumbiji)

  Km 297

  Km 40 kwa saa

  Kwa taarifa hizi za mwenendo wa mgandamizo huo mdogo, ingawa kwa sasa upo katika ardhi ya Msumbiji na hautarajiwi kutua katika ardhi ya Tanzania, lakini ni wazi kuwa siyo mbali sana na mpaka waTanzania, hivyo ni matarajio kuwa mifumo ya hali ya hewa katika maeneo mengi ya nchi yetu itaendelea kuendeshwa na mgandamizo huu. Aidha, vipindi vya mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali vinaweza kujitokeza kufuatana na mchango wa mgandamizo huu katika kuvuta unyevunyevu kutoka magharibi kuelekea katika nchi yetu.

  Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa mgandamizo mdogo wa hewa (Depression Ex-Kenneth) uliopo kaskazini-mashariki mwa nchi ya Msumbiji pamoja na mwenendo wa mifumo mingine ya hali ya hewa kwa ujumla na itaendelea kutoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.

  USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza. Aidha izingatiwe kuwa hatua za kujiandaa kukabiliana na majanga zinatumia gharama ndogo ikilinganishwa na gharama ambayo ingetumika kukabili na kurejesha hali.

 • Weather by Region

  © 2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.