Habari

Imewekwa: Jul, 20 2021

NAIBU SPIKA: VYOMBO VYA HABARI TENGENI MUDA WA KUTOSHA KURUSHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

NAIBU SPIKA: VYOMBO VYA HABARI TENGENI MUDA WA KUTOSHA KURUSHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

Dar es Salaam; Tarehe 09 Julai, 2021;

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson (MB) ametoa wito kwa vyombo vya habari kutenga muda wa kutosha wa kurusha taarifa za hali ya hewa mara kwa mara ili kusaidia wananchi kuzipata kwa wakati na kuzitumia kwa ufanisi zaidi. Aidha, alieleza kuwa kutokana na muda wa habari ya hali ya hewa kuwa mfupi, taarifa zinatolewa kwa ujumla na kwa ufupi, kitu ambacho kinaweza kuathiri matumizi yake.

“Nitoe wito kwa vyombo vya habari kuangalia namna ambavyo watakuwa wanazitumia taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kuzitoa mara kwa mara ili kutusaidia sisi wananchi kujiandaa na kufanya maamuzi sahihi katika mipango yetu, tuangalie kama vyombo vingine vya habari vya mataifa ya nje, ukifungua kila wakati unaangalia hali ya hewa”Alisema Dkt. Tulia wakati alipotembelea Makao Makuu ya TMA.

Aliendelea kusema kuwa, alichojifunza katika ziara yake fupi katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, ni kuwa taarifa zipo, lakini kwa ajili ya muda mfupi basi Mamlaka inalazimika kuziweka katika huo muda mfupi.

Kwa upande mwingine, alito wito kwa wananchi kuitembelea Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ili kujifunza masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna taarifa za hali ya hewa zinavyochakatwa kitaalamu hadi kumfikia mtumiaji.