Habari

Imewekwa: Oct, 05 2021

MHE. WAITARA AMEITAKA TMA KUWEKEZA KATIKA KUBORESHA MAZINGIRA YA CHUO CHA HALI YA HEWA.

MHE. WAITARA AMEITAKA TMA KUWEKEZA KATIKA KUBORESHA MAZINGIRA YA CHUO CHA HALI YA HEWA.

Dar es Salaam; Tarehe 04 Oktoba, 2021;

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi(Sekta ya Uchukuzi), Mhe. Mwita Mwikwabe Waitara (MB) ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuwekeza zaidi katika kuboresha mazingira ya chuo cha hali ya hewa kilichopo Kigoma.

Hayo yalizungumzwa katika ziara ya Mhe. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 04/10/2021. Lengo la ziara hiyo ni kuifahamu TMA, kazi wanazofanya na kutambua changamoto za kiutendaji ili kuweza kufanya maboresho stahiki.

“Nilipokwenda Chuo cha hali ya hewa Kigoma niliona mazingira yake sio mazuri pamoja na kuwa Chuo hicho kipo katika ukarabati kinahitaji kiwe na mazingira mazuri kutokana na kuwa ndio chou pekee kinachotoa mafunzo ya awali ya hali ya hewa hapa nchini. Nafikiri mwenyekiti wa bodi na Mkurugenzi Mkuu mnapaswa kuwekeza pale” Alizungumza Mhe. Waitara.

Mheshimiwa Naibu Waziri aliongezea kuwa Mamlaka inajukumu kubwa kwasababu taarifa za hali ya hewa zinatumika katika sekta zote za maendeleo hapa nchini. Mwekezaji akitaka kuwekeza lazima afuatilie taarifa za hali ya hewa ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha aliwapongeza TMA kwa kazi nzuri wanazozifanya na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa weledi wakijua kwamba kazi wanazozifanya zina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini. “Nawapongeza kwa kuboresha huduma za hali ya hewa hapa nchini na pia kuifanya Tanzania iendelee kung’ara katika Nyanja za kimataifa kwenye sekta ya hali ya hewa. Aliongeza Mhe. Waitara.

Mhe. Waitara aliahidi kwamba katika utaratibu wa kuboresha maslahi ya watumishi kama alivyoahidi Mhe. Rais watumishi wa TMA wataboreshewa Maslahi yao ili waweze kufanyakazi kwa ufanisi.

Awali, wakati akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi kupitia taarifa yake fupi alisema kuwa Mamlaka imeanza kuifanyia kazi changamoto ya vifaa ambapo Serikali imeendelea kutenga fedha kwaajili ya ununuzi wa vifaa vya hali ya hewa. Changamoto ya maslahi duni nayo pia imeanza kufanyiwa kazi ambapo ‘Job Evaluation’ imefanyika kwa kutumia Chuo cha Utumishi wa Umma na mapendekezo ya mishahara stahiki kwa wafanyakazi yamewasilishwa katika Mamlaka husika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi alishukuru Serikali, “Napenda kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwani imeendelea kuiwezesha Mamlaka kuwa na vitendea kazi vya kisasa na wataalamu bingwa ambao wanapatiwa mafunzo mara kwa mara kwa lengo la kuwaongeza ujuzi”. Alisema Dkt. Kijazi. Aliongeza kusema “Nichukue fursa hii adhimu kuishukuru Serikali yetu kupitia Wizara kwa kutupatia Rada nyingine mbili ambazo ukamilikaji wake utapelekea kufikiwa kwa malengo ya muda mrefu ya kuwa na Rada 7 za hali ya hewa kwa nchi nzima”.

Alimalizia kwa kumhakikisha Mhe. Naibu Waziri kwamba maelekezo yote aliyoyatoa hususan uboreshaji wa Miundombinu ya Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma yatawekewa mpango mkakati wa utekelezaji.