Habari

Imewekwa: Sep, 23 2021

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) YAPATA VIFAA VIPYA VYA KUPIMA HALI YA HEWA YA ANGA LA JUU (UPPER AIR)

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) YAPATA VIFAA VIPYA VYA KUPIMA HALI YA HEWA YA ANGA LA JUU (UPPER AIR)

Dar es Salaam; Tarehe 13/09/2021

Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limeipatia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)vifaa vipya vya kupima hali ya hewa ya anga la juu (upper air).Vifaa hivyo vimetolewa kwa TMA ikiwa ni msaada chini ya utekelezaji wa program ya WMO ya kuboresha huduma za hali ya hewa kwa Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki (EAC) zinazozunguka eneo la Ziwa Viktoria, iitwayo “HIGH impact Weather lAke SYstems (HIGHWAY)”.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na: mtambo wa kuzalisha gesi ya haidrojeni (Hydrogen gas Generator); radiosonde; Maputo maalumu ya kupima hali ya hewa ya anga za juu (weather balloons);program za kompyuta (computer softwares)na mavazi maalumu kwa ajili ya usalama. Vifaa hivyo vimefungwa tarehe 7 Septemba, 2021 katika kituo cha kupima hali ya hewa ya anga la juu (Upper Air Station) kilichopo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa MwalimuJulius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA). Aidha, zoezi la ufungaji wa vifaa hivyo lilienda sambamba na mafunzo kwa wataalamu.

Ufungwaji wa vifaa hivyo umewezesha kuhuisha kituo hichokuwa cha kisasa zaidi baada ya mitambo ya awali kuwa chakavu. Kituo hicho kwa sasa kitaendelea na shughuli zake za kupima hali ya hewa ya anga la juu kama kawaida.Uhuishaji wakituo hicho utawezesha kupima takwimu za hali ya hewa ya anga la juu, ambazo ni muhimu sana katikakutoa utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi mbalimbali hususan usalama na usafiri wa anga nchini.

Programu hiyo ya HIGHWAY ilitekelezwa nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia Septemba, 2017, ambapo miongoni mwa shughuli zake zilihusisha pia uhuishaji wa kituo hicho cha kupima hali ya hewa ya anga la juu katika uwanja wa JNIA. Msaada wa vifaa vilivyotolewa na WMO ni sehemu ya utaratibu wa Shirika hilo ikiwa ni mrejesho kwa Nchi Wanachama kutokana na michango inayotolewa na Serikali za Nchi Wanachama kupitia ada ya uanachama kwa Shirika hilo.