|
RANET ni kifupi cha RAdio na InterNET kwa ajili ya mawasiliano ya taarifa za kijamii hususan taarifa za hali ya hewa zikiwemo utabiri wa misimu ya mvua na tahadhari za hali mbaya ya hewa. Mojawapo ya mifano ya taarifa mbaya za hali ya hewa ni pamoja na ukame, mafuriko na vimbunga.
Mradi wa RANET ulibuniwa na Shirika la Hali ya Hewa la Marekani linalohusika na uchunguzi wa mienendo ya bahari na anga (NOAA). Lengo la mradi huu ni kusambaza na kufikisha taarifa za hali ya hewa na nyingine muhimu za kijamii kwa wananchi waishio katika maendeleo ya kisasa hususani vijijini katika bara la Afrika, Asia na Pasifiki.
Mradi huu wa RANET ambao ulipelekwa Afrika Magharibi kwa mara ya kwanza mwaka 2001 umekwishaonyesha mafanikio makubwa katika baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Niger, Uganda, Kenya, Msumbiji na Zambia. RANET ni kifaa kisicho na gharama kubwa kinachotumia teknolojia ya redio na mtandao (internet) kwa pamoja kama inavyoonyeshwa kwenye picha. Vyote hutumika kwa kupokea taarifa zinazoakisiwa na Satellite za mawasiliano angani.
 |
 |
| Redio |
Ranet Receiver |
Japo uchumi wa Tanzania hutegemea sana kilimo cha mvua, wakulima waishio vijijini hawapati taarifa za hali ya hewa na hali ya mazingira, matarajio na mabadiliko ya misimu ya mvua ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya mifugo, afya, kilimo, utunzaji wa misitu na vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu. Hivi sasa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, TMA inasambaza taarifa zake kwa kutumia televisheni, magazeti, redio na tovuti ya Mamlaka. Hata hivyo njia hizo hazikidhi mahitaji kwa vile taarifa`kupitia vyombo hivi vya habari haziwafikii wananachi huko vijijini na kwa wakati.
RANET hapa nchini inatarajiwa kuwa mojawapo ya teknolojia rahisi zitakazosaidia kukidhi upatikanaji wa taarifa mbalimbali za kijamii katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi yakiwa ni pamoja na vijijini. Teknolojia hiyo itawezesha wananchi vijijini kupata na kutumia taarifa za hali ya hewa ambazo zitawasaidia katika kuendeleza shughuli zao kama vile kilimo na kupunguza athari zitokanazo na majanga.
TMA tayari ilishaanza mkakati wa kusambaza teknolojia hii rahisi kwa kuendesha semina ya mafunzo ya RANET kwa baadhi ya wawakilishi wa wananchi waishio vijijini kutoka mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga na Arusha. Mafunzo hayo yaliyofanyikia mjini Morogoro kuanzia tarehe 8 hadi 9 mwezi Februari 2007 ambayo yalikuwa ya mafanikio na tayari mwezi Julai 2007, TMA ilinunua na kufunga RANET ishirini kwa baadhi ya wadau waliopata mafunzo hayo. Maeneo yaliyofungiwa RANET ni pamoja na Monduli (Arusha), Muheza na Mazingara (Tanga), Msata (Bagamoyo), Ilonga na Mgeta (Morogoro) Ni matarajio ya TMA kuwa kwa kushirikiana na taasisi na mashirika mbalimbali ya serikali na ya binafsi, mradi huu utakua hatua kwa hatuaa, hadi kuenea nchi nzima.

Semina ya mafunzo ya RANET, Morogoro 8-9 Februari 2007
Picha zifuatazo zinaonyesha ufungaji wa RANET katika maeneo yaliyotajwa:

Chuo cha VETA - Msata, Bagamoyo

Shule ya msingi Mazingara, Tanga

Chuo cha utafiti cha kilimo, Ilonga, Kilosa

NGO ya TUINECATA Mgeta, Morogoro

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Muheza, Tanga (misitu na uvuvi, Bomani) Tanzania (MVIWATA), Monduli, Arusha |