Machapisho

UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA (MAM) 2020

Pakua

Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Machi-Mei (Masika) 2020

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Machi – Mei, 2020, ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii; Nishati na Maji; Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Mambo muhimu katika taarifa hii ni:-

i. Mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mashariki mwa mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.
ii. Maeneo ya mkoa wa Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
iii. Mvua za nje ya msimu zinazoendelea kunyesha katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, hususan yaliyopo katika pwani ya kaskazini zinatarajiwa kuendelea na kuungana na msimu wa mvua wa Masika 2020.


Athari zinazotarajiwa:


i. Mvua za kutosha katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, zinatarajiwa kunufaisha uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo yale yanayostahimili unyevunyevu mwingi ardhini kama vile mpunga. Aidha, uwepo wa malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo na wanyamapori vinatarajiwa.
ii. Milipuko ya magonjwa na wadudu waharibifu vinaweza kujitokeza kutokana na hali ya unyevunyevu na kutuama kwa maji.
iii. Uchimbaji wa madini ufanyike kwa kuzingatia utabiri uliotolewa kwani ongezeko la maji katika udongo linaweza kusababisha maporomoko ya ardhi hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
iv. Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua stahiki kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali pakua