Habari

Imewekwa: Dec, 14 2020

WACHIMBAJI MADINI WATAKIWA KUTUMIA TAARIFA MAHSUSI ZA HALI YA HEWA KUONGEZA TIJA NA UFANISI.

WACHIMBAJI MADINI WATAKIWA KUTUMIA TAARIFA MAHSUSI ZA HALI YA HEWA KUONGEZA TIJA NA UFANISI.

Dodoma; Tarehe 08 Disemba, 2020;

Wadau kutoka sekta ya madini nchini wametakiwa kutumia taarifa mahsusi za hali ya hewa ili kuweza kuongeza tija, ufanisi na usalama katika shughuli zinazohusiana na utafutaji, uchimbaji madini na uendeshaji wa migodi.

Matakwa hayo yalitolewa na mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Madini kuhusu Umuhimu wa Huduma za Hali ya Hewa, Mhandisi, Aron Kisaka ambaye alifungua mkutano huo akimwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi).

“Taarifa sahihi za hali ya hewa zikiwafikia wachimbaji kwa wakati, zitasaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na kupanga mipango ya kukabiliana na majanga ndani ya sekta yatokanayo na hali mbaya ya hewa kama vile maporomoko ya udongo”. Alizungumza Mhandisi Kisaka.

Aidha, Mhandisi Kisaka aliwataka washiriki wa mkutano huo kutoka na uelewa chanya kuhusu sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 hususan uhusiano wake na sekta ya madini.

Awali, wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) aliwashukuru wadau kwa kuitikia mwaliko na kueleza kuwa Mamlaka inatoa huduma mahsusi kwaajili ya sekta mbali mbali nchini ikiwa pamoja na sekta ya madini, hata hivyo wadau katika sekta ya madini bado hawazitumii ipasavyo huduma hizo. Dkt. Kijazi aliomba washiriki wa mkutano kutumia fursa ya mkutano huo kuelewa huduma mbali mbali zinazotolewa na TMA na kuweka mkakati wa kuzitumia.

“Mkutano huu utakuwa ni fursa muhimu ya kujengeana uelewa kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya madini na faida zitakazopatika endapo huduma hizo zitatumiwa ipasavyo”. Alisema Dkt. Kijazi

Naye, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Bw. Robert Sunday alielezea umuhimu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kukutana na wadau wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini. Alifafanua kwamba kwa vile Tanzania kupitia Dkt.Kijazi inashika nafasi ya makamu wa tatu wa rais wa WMO ni muhimu nchi yetu ikawa kielelezo katika utumiaji wa taarifa za hali ya hewa katika sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya madini. Aidha, alimshukuru mgeni rasmi kwa hotuba nzuri yenye lengo la kujenga na aliwashukuru washiriki wa mkutano huo hususan wadau wa sekta ya madini kwa ushiriki wao.

Kwa upande wa mwakilishi wa wachimbaji madini, Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Tanzania (FEMATA) na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Bw. Haroun Kinega aliishukuru TMA kwa kushirikiana na Tume ya Madini kuandaa mkutano huo muhimu ambao utaleta mwanga kwa wachimbaji wote kwa ujumla juu ya matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa. Alikiri kwamba taarifa za hali ya hewa ni za muhimu sana katika sekta ya madini.

Mkutano huu uliofanyika katika ukumbi wa LAPF, Dodoma, Tarehe 08 Disemba 2020, umewakutanisha wadau mbalimbali katika sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wakubwa, wakati na wadogo, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Madini, Tume ya Madini, NEMC na TMA.