Habari

Imewekwa: Feb, 13 2020

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

“Mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mashariki mwa mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara”. Alisema Dkt. Kijazi

Aliendelea kwa kuyataja maeneo ya mkoa wa Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro kuwa yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Aidha, Dkt. Kijazi alifafanua kuhusu mvua za nje ya msimu zinazoendelea katika maeneo yanayopata mvua za Masika hususan maeneo yaliyopo katika pwani ya kaskazini, mvua hizo zinatarajiwa kuendelea na kuungana na msimu wa mvua wa Masika 2020.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua stahiki kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa taarifa zaidi tembelea: http://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast