Habari

Imewekwa: Jun, 09 2020

TANZANIA YAONGOZA MKUTANO WA KUWIANISHA SHUGHULI ZA UTOAJI HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA UKANDA WA SADC.

TANZANIA YAONGOZA MKUTANO WA KUWIANISHA SHUGHULI ZA UTOAJI HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA UKANDA WA SADC.

Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamefanya mkutano wa kuwianisha shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa katika Ukanda wa SADC (Harmonizing SADC Strategy and Action Plan on Meteorology).

Mkutano huo ulifanyika tarehe 4 Juni 2020 kwa njia ya mtandao (videoconference) chini ya Uenyekiti wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapoMkurugenzi Mkuu waTMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliongoza mkutano huo.

Akiwasilisha hotuba yake fupi ya ufunguzi, Dkt. Kijazi alisema kuwa dhumuni kuu la mkutano huo ni kuwianisha shughulizautoaji wa huduma za hali ya hewa katika Ukanda wa SADC ili zichangie ipasavyo katika kutatua changamoto zasekta ya hali ya hewa katika Ukanda wa SADC kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika Nchi Wanachama. Dkt. Kijazi alizitaja baadhi ya changamoto zinazokabili sekta ya hali ya hewa kuwa ni pamoja na uhaba wa miundombinu ya kupima hali ya hewa; kuchakata takwimu za hali ya hewa; na kubadilishana takwimu za hali ya hewa.

Dkt. Kijazi aliendelea kueleza kwamba, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Nchi Wanachama kuboresha huduma za hali ya hewa, utatuzi wa changamoto hizo unahitaji pia juhudi za pamoja za wadau na taasisi zote husika ili kuwianisha shughuli za huduma ya hali ya hewa za Kikanda.

“Licha ya jitihada zilizofanywa na Nchi wanachama katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, bado kuna changamoto nyingi.Kama sehemu ya utatuziwa changamoto hizi, mkutano huu utajadili namna ya kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa za Kikanda” alisema Dkt. Kijazi na kuwaomba wajumbe kushiriki kikamilifu na kutoa maoniyatakayofanikisha uwianishaji wa shughuli hizo.

Akitoa maelezo ya awali kuhusiana na mkutano huo, Afisa Mwandamizi wa Programu ya Hali ya Hewa katika Secretarieti ya SADC, Dkt. Prithiviraj Booneeady, alisema hatua ya kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa ni takwa laItifaki ya SADC ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport, Communication and Meteorology) unaozitaka Nchi Wanachama kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa ili kuwezesha ushirikiano wa Kikanda na kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika utoaji wa huduma za hali ya hewa.Kwa mujibu wa Dkt. Booneeady, hatua hiyo itasaidia juhudi za pamoja katika kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika kukabiliana na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa.

Mada zilizowasilisha katika mkutano huo ni pamoja na zinazohusiana na programu za Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) katika ukanda wa SADC; Programu za Secretarieti ya SADC zinazohusiana na sekta ya hali ya hewa; Programu za Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa Kusini mwa Afrika (SADC MASA). Mkutano ulijadili shughuli hizo na kutoa mapendekezo. Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kurejewa upya kwa Itifaki ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport, Communication and Meteorology) ili ukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya hali ya hewa.