Habari

Imewekwa: Jun, 19 2020

KUPATWA KWA JUA TAREHE 21 JUNI, 2020.

KUPATWA KWA JUA TAREHE 21 JUNI, 2020.

Dar es Salaam, 19 Juni 2020:

Hali ya kupatwa kwa Jua ni tukio linalohusisha kivuli cha mwezi kuangukia juu ya uso wa Dunia ambapo katika maeneo yaliyo ndani ya kivuli hicho Jua huonekana likifunikwa na Mwezi kwa kipindi cha saa chache.

Hali hii ya kupatwa kwa Jua Kipete, inatarajiwa kutokea siku ya Jumapili, Tarehe 21 Juni 2020 katika baadhi ya maeneo ya Bara la Afrika .Kupatwa huku kwa jua kutaanzia nchi za Afrika ya Kati, kukatisha ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania hususani maeneo ya Dar es Salaam, Bukoba, Arusha na Dodoma na kuelekea kusini mwa rasi ya Uarabuni, kaskazini mwa bara la Hindi na kusini mwa China na hatimaye kuishia katika Bahari ya Pasifiki. Tukio hili litaanza saa 12:50 asubuhi, kufikia kilele saa 01:45 na kumalizika saa 02:50 asubuhi kwa eneo la Tanzania.

Aidha, sehemu ya Jua itakayofunikwa na Mwezi wakati wa kilele cha kupatwa kwa Jua kipete itatofautiana baina ya eneo na eneo. Maeneo yaliyo ndani ya njia ya kupatwa kwa Jua yataona kupatwa kwa Jua kwa kiwango kikubwa zaidi ikilinganishwa na maeneo yaliyo mbali zaidi na njia hii. Kwa kuwa Tanzania inaangukia katika eneo la mbali zaidi na njia hiyo, kupatwa kwa Jua kutakuwa kudogo zaidi ambapo kufunikwa kwa Jua hakutazidi asilimia 50%.

Kuna aina mbili za kupatwa kwa Jua; kupatwa kwa Jua kikamilifu ambapo mwezi huzuia kabisa mwanga ya Jua kufika katika Dunia na aina ya pili, kupatwa kwa Jua kipete, Mwezi huzuia sehemu tu ya mwanga wa Jua, hivyo kutengeneza umbo la pete ya mwanga wa jua angani.

Hali ya Hewa

Kwa ujumla hakuna athari zozote kubwa zinazotarajiwa katika mifumo ya hali ya hewa kutokana na tukio hili la kupatwa kwa Jua.

Hata hivyo, upo uwezekano wa kuongezeka kwa muda wa baridi katika nyakati za asubuhi hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi, kutokana na maeneo hayo kuwa karibu na njia ya kupatwa kwa Jua na kuchelewa kwa mwanga wa Jua ambao husababisha uwepo wa joto.

Kwa upande mwingine, uwezekano wa kuona kupatwa kwa Jua unaweza kupungua katika baadhi ya maeneo ya kaskazini na yale ya kati mwa nchi hususan nyakati za asubuhi kutokana na matarijio ya hali ya mawingu.

Ushauri

Wananchi wanashauriwa kutoangalia Jua moja kwa moja bila kutumia vifaa vinavyoshauriwa na wataalamu ili kuepuka athari za miale ya Jua.

Mamlaka ya hali ya hewa inaendelea kufuatilia na itatoa taarifa za mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika hali ya hewa kulingana na tukio hili la kupatwa kwa jua.