Habari

Imewekwa: Dec, 22 2020

SERIKALI YAKABIDHIWA RADA YA TATU YA HALI YA HEWA ILIYOPO MTWARA.

SERIKALI YAKABIDHIWA RADA YA TATU YA HALI YA HEWA ILIYOPO MTWARA.

Dar es Salaam; Tarehe 18 Disemba, 2020;

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhiwa rasmi rada ya tatu ya hali ya hewa ambayo imefungwa katika Kilima cha Mbae, Mtwara. Makabidhiano hayo yamefanyika baini ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na mzabuni Enterprise Electronics Corporation (EEC) kutoka Marekani. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye kituo kikuu cha utabiri cha TMA, Tarehe: 18 Disemba 2020 na yalishuhudiwa na mwakilishi wa mwenyekiti wa bodi ya TMA.

“Serikali imekamilisha upatikanaji wa rada ya tatu ya hali ya hewa, Rada ya kisasa ni moja ya mitambo michache iliyofungwa Duniani hivyo tunauhakika wa kupata taarifa za hali ya hewa za uhakika na kwa wakati” alisema hayo Mhandisi Aron Kisaka, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi)wakati wa makabidhiano hayo.

Aidha aliongeza kwa kuishukuru Enterprise Electronics Corporation (EEC) kwa ushirikiano waliouonesha hata kufanikisha ufungwaji wa rada hiyo ya kisasa hapa nchini na akawataka kuendelea kutoa ushirikiano katika kipindi chote ambacho rada hiyo itakuwa kwenye warranty. Aidha alieleza kuwa uzinduzi rasmi wa Rada ya Mtwara utafanyika hivi karibuni baada ya kumalizika kipindi cha majaribio.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru serikali kwa jitihada zake za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuendelea kukamilisha ahadi ya kufungwa Rada saba nchi nzima, hii ikiwa rada ya tatu kufungwa na tayari rada zingine mbili zitakazofungwa Mbeya na Kigoma ziko katika hatua za mwisho za matengenezo.

Naye mwakilishi wa Enterprise Electronics Corporation (EEC) kutoka Marekani Bw. Edwin Kasanga aliihakikishia Serikali kuwa wataendelea kutoa ushirikiano wa dhati ili kuhakikisha miradi inayoendelea inakamilika kwa wakati kulingana na makubaliano ya mikataba. Aidha, akisoma ujumbe Bw. Chris Goode ambaye ni Rais wa EEC, Mhandisi James Youngblood alieleza kuwa pamoja na janga kubwa la virusi vya COVID19 kampuni yake ilipambana kufanikisha makubaliano ya mkataba kwani ilitambua umuhimu wa rada hiyo katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa Tanzania.

Rada ya Mtwara ni rada ya tatu kufungwa nchini, ikiwa ni moja kati ya rada saba zinazotarajiwa kukamilisha mtandao wa rada hapa nchini.