Habari

Imewekwa: Jan, 10 2020

KUPATWA KWA MWEZI TAREHE 10 – 11 JANUARI 2020

KUPATWA KWA MWEZI TAREHE 10 – 11 JANUARI 2020

Hali ya kupatwa kwa mwezi ni tukio la aina yake linatokea pale ambapo Dunia inapita kati ya Jua na Mwezi, hivyo dunia husabisha kivuli katika uso wa mwezi. Muda wa kufunikwa kabisa ni dakika chache tu katika eneo husika.

Kupatwa kwa mwezi kunatokea wakati dunia, mwezi na jua vinapokaa
kwenye mstari mmoja mnyoofu. Kutokana na hali hiyo kupatwa kwa
mwezi kwa maeneo yaliyo mengi kunaonekana kwa watu wengi kama
kupungua kwa mng’aro wa mwezi.

Maelezo ya Kisayansi

Wanasayansi wanaelezea kupatwa kwa mwezi kama tukio linalotokea
na kuonekana katika namna tofauti tofauti mfano; ni kupatwa kwa
mwezi kikamilifu (Umbra) hali ambayo huonekana pale hutokea giza
katika uso wa mwezi hutokea kwa kipindi kifupi.

Aina ya pili ni kupatwa kwa mwezi kisehemu (Penumbra); hii hutokea
wakati dunia inaposababisha kivuli hafifu katika uso wa mwezi.

Tukio la kupatwa kwa mwezi la 10 hadi 11 Januari 2020 ni la kupatwa
kwa mwezi kisehemu (Penumbra). Tukio hili litaonekana katika nusu ya Dunia hususan maeneo ambayo tarehe hii utakuwa usiku (Ulaya, Asia, Australia na Afrika).

Kwa hapa nchini hali hiyo inatarajiwa kuonekana katika sehemu yote
ya nchi kuanzia saa 2:07 tarehe 10 hadi saa 6:17 usiku wa kuamkia
tarehe 11/01/2020

Athari zake kwa Hali ya Hewa.

Kwa ujumla hakuna athari zozote kubwa zinazotarajiwa kutokana na
hali hiyo. Hata hivyo, upo uwezekano wa kuongezeka kwa kina cha
maji katika bahari wakati maji kujaa. Hii inasababishwa na mvutano kati ya mwezi na maji katika bahari.

Hali ya anga inatarajiwa kuwa yenye mawingu kidogo. Hii itatoa
nafasi nzuri ya kuonekana kwa tukio hilo kwa macho.

Upekee wa tukio la kupatwa kwa Mwezi.

Tukio hili hutokea au kujirudia mara chache sana katika eneo husika.
Hii ndio sababu kwa watu wa eneo husika na wanasayansi limekuwa ni
tukio muhimu na la kipekee.

Mamlaka ya hali ya hewa inaendelea kufuatilia na itatoa taarifa za mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika hali ya hewa kulingana na tukio hili la kupatwa kwa mwezi.