Habari

Imewekwa: Nov, 28 2019

BODI MPYA YA TMA YATAKIWA KUSIMAMIA JUKUMU JIPYA LA TMA LILILOAINISHWA KATIKA SHERIA.

BODI MPYA YA TMA YATAKIWA KUSIMAMIA JUKUMU JIPYA LA TMA LILILOAINISHWA KATIKA SHERIA.

Dar es Salaam, Tarehe 28/11/2019: “Mkasimamie vizuri jukumu jipya la Mamlaka la usimamizi wa huduma za hali ya hewa nchini kama ilivyoainishwa katika sheria”. Alizungumza Mhe. Mhandisi. Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wakati akizindua rasmi Bodi mpya ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Mhe. Kamwelwe aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha kuwa inasimamia kwa umakini utekelezaji wa sheria iliyoanzisha TMA. Aidha alisisitiza Bodi kuhakikisha mapato ya Mamlaka yanaongezeka kwa kuhakikisha ukusanyaji wa Mapato unazingatia vyanzo vyote ambavyo huduma za hali ya hewa zinatumika kibiashara, sambamba na hayo aliitaka Bodi hiyo pia kuboresha maslahi ya watumishi ili kuondoa wimbi la watumishi kuhamahama kwa kutafuta maslahi bora katika taasisi nyingine nje na ndani ya nchi.

Naye mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Buruhani Nyenzi alitoa shukrani za dhati kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwateua yeye mwenyewe kuwa Mwenyekiti na Dkt. Makame Omar Makame kuwa Makamu Mwenyekiti katika kuongoza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Aidha Dkt. Nyenzi alisema anatambua kuwa majukumu waliyopewa ni mazito na yanahitaji uwajibakaji na kufanya kazi kwa kasi, weledi na nguvu.

“Nafasi hii ni nyeti na majukumu tuliyokabidhiwa mimi pamoja na wajumbe wenzangu wa Bodi ni mazito na yanayohitaji uwajibakaji na kufanya kazi kwa kasi, weledi na nguvu ili kuweza kuendana na maono makubwa ya Mh. Rais, John Pombe Magufuli”. Alisema Dkt. Nyenzi.

Kwa upande mwingine wakati akitoa taarifa fupi ya TMA, Dkt. Agnes Kijazi, alifafanua shughuli zinazofanywa na TMA pamoja na mafanikio ya Mamlaka ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mifumo mbalimbali (software) za kuboresha utendaji kazi wa TMA zilizobuniwa na wataalam wa ndani ya Mamlaka na hivyo kupunguza gharama kubwaza uendeshaji.

Awali, mmoja wa wajumbe wa Bodi ambaye pia alimwakilisha Katibu Mkuu (Uchukuzi) Mhandisi. Aron Kisaka alitoa maelezo mafupi ya utambulisho wa Bodi na kutoa shukrani kwa mhe. Rais pamoja na Mhe. Waziri kwa uteuzi walioufanya wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi.

Uzinduzi wa Bodi mpya umefanyika katika ukumbi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dar es Salaam. Wajumbe wa Bodi hiyo ni Dkt. Buruhani Nyenzi (Mwenyekiti), Dkt. Makame Omar Makame (Makamu Mwenyekiti), Kapt. Large Temba (Mjumbe), Bw. Robert Sunday (Mjumbe), Bi. Marystella Mtalo (Mjumbe), Bi. Jane Kikunya (Mjumbe), Mhandisi. Aron Kisaka (Mjumbe) na Dkt. Agnes Kijazi (Katibu).