Habari

Imewekwa: Oct, 15 2019

TMA YAHIMIZA WAKAZI WA PEMBA KUTUMIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KATIKA SEKTA YA KILIMO.

TMA YAHIMIZA WAKAZI WA PEMBA  KUTUMIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KATIKA SEKTA YA KILIMO.

Kuanzia Tarehe 10 hadi 16 Oktoba 2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inashiriki katika maonesho ya siku ya chakula Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwe kisiwani Pemba ambapo wataalamu wa hali ya hewa wameendelea kutoa elimu kwa wakazi kisiwani Pemba, juu ya umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta ya kilimo.

Meneja wa hali ya hewa kituo cha Pemba Bi. Bishara Mdowe aliongea na wananchi wa Pemba kupitia vyombo vya habari na kuwakumbusha kuwa hivi sasa dunia imekumbwa na mabadiliko ya tabia nchi, hivyo kuwataka kuhacha kufanya shughuli za kilimo kwa mazoea ili kuepusha hasara zisizo za lazima na badala yake waanze kutumia taarifa za hali ya hewa ili kufanya kilimo chenye tija kitakachokuza uchumi wao pamoja na Taifa kwa ujumla. “Ninawakumbusha wananchi wa pemba, hivi sasa Dunia imekumbwa na mabadiliko ya tabia nchi, hivyo tuache kufanya shughuli za kilimo kwa mazoea, ninawahimiza kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ili kuepusha hasara zisizo za lazima”.

Aidha kwa upande wa wageni waliotembelea katika banda la TMA lililopo katika maonesho hayo akiwemo afisa mdhamini Wizara ya Uchukuzi, Mawasiliano na Usafirishaji - Pemba ndugu. Hamad Baucha walionesha kufurahishwa na namna elimu inavyotolewa na kuomba elimu iendelee kutolewa mara kwa mara zaidi kupitia vipindi vya redio na runinga. Kauli mbiu ya maonesho hayo ni "Matendo yetu ndiyo Hatma yetu, Lishe Bora kwa Ulimwengu usio na Njaa"

Kwa matukio zaidi katika picha tembelea: https://meteotz1950.blogspot.com/2019/10/tma-yahimiza-wakazi-wa-pemba-kutumia.html