Habari

Imewekwa: Apr, 08 2020

DKT. KIJAZI: MWAKA 2019 ULIREKODI KIASI CHA MVUA NYINGI TANGU MWAKA 1970.

DKT. KIJAZI:  MWAKA 2019 ULIREKODI KIASI CHA MVUA NYINGI TANGU MWAKA 1970.

Dar es Salaam, Tarehe 08/04/2020:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa ripoti ya tathimini ya hali ya hewa ya Tanzania kwa mwaka 2019. Uzinduzi wa ripoti hiyo ulifanyika wakati wa kikao cha Bodi ya TMA kilichofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya TMA.

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi alisema mwaka 2019 umechukua nafasi ya nne kwa kurekodi kiasi cha mvua nyingi tangu mwaka 1970.

“Kiwango cha mvua nchini kwa mwaka 2019 kilikuwa ni wastani wa milimita 1283.5 sawa na asilimia 125 ya wastani wa mvua ya muda mrefu (1981-2010), kiwango hiki ni zaidi ya wastani wa mvua ya muda mrefu kwa milimita 256.5. Katika historia, mvua hii imechukua nafasi ya nne kwa wingi kati ya miaka iliyopata mvua nyingi zaidi tangu mwaka 1970 ambapo miaka iliyokua na mvua nyingi zaidi tangu mwaka 1970 ni 1982, 1997 na 2006”. Alisema Dkt. Kijazi

Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa joto la nchi limeendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu kuanzia mwaka 1995, ambapo joto la usiku limeongezeka zaidi ilikilinganishwa na joto la mchana. Pamoja na hayo taarifa za ripoti zitolewazo zimekuwa zikichangia ripoti za tathimini ya hali ya hewa ya dunia zinazoandaliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Vilevile Dkt. Kijazi alitoa wito kwa wadau wa sekta mbalimbali kutumia taarifa zilizopo kwenye ripoti hiyo kwaajili ya mipango ya maendeleo ya kiuchumi na jamii kama vile kilimo, ujenzi, maendeleo ya viwanda n.k

Awali wakati akitoa maelezo ya jumla, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema kuwa, ripoti hizi zimekuwa zikitolewa tokea mwaka 2011 hadi 2019 na lengo ni kukuza ufahamu na uelewa kwa jamii, wadau na watoa maamuzi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi. “Tathmini za ripoti hizi huonesha taarifa za kina za uchambuzi wa hali ya hewa na athari zake na kuziweka katika mtazamo wa kihistoria”. Alisema Dkt. Chang’a

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt. Buruhani Nyenzi aliipongeza Menejimenti ya TMA kwa kutoa taarifa hiyo kwani ilielezwa kwamba ni nchi mbili tu Afrika ambazo zinatoa taarifa hizo ikiwemo Tanzania na Ivory Coast