Habari

Imewekwa: Nov, 05 2019

DKT. KIJAZI AUTANGAZA MLIMA KILIMANJARO KATIKA MKUTANO WA WMO UNAOHUSU MAENEO YENYE MILIMA YENYE VILELE VIREFU DUNIANI.

DKT. KIJAZI AUTANGAZA MLIMA KILIMANJARO KATIKA MKUTANO WA WMO UNAOHUSU MAENEO YENYE MILIMA YENYE VILELE VIREFU DUNIANI.

Geneva, Tarehe 29/10/2019: Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shiriki la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi ameshiriki katika mkutano wa kimataifa unaohusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye maeneo yenye milima yenye vilele virefu duniani, uliofanyika makao makuu ya WMO mjini Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 29-31 Oktoba 2019.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa shirika la Hali ya Hewa Duniani Prof. Petteri Taalas, Dkt. Kijazi katika nafasi yake kama makamu wa tatu wa Rais wa Shirika hilo alishiriki katika hafla fupi ya ufunguzi wa mkutano huo. Aidha kama mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa Dkt. Kijazi alishiriki katika jopo la wataalam (Panel) ambapo alipata fursa ya kuwasilisha mada iliyohusu Mlima Kilimanjaro.

Mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu katika bara la Afrika, pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea Duniani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua kuhakikisha inahifadhi mazingira katika eneo la mlima huo kwa kuhifadhi sehemu ya mlima huo kama ‘National Park’.

“Pamoja na kuona mandhari nzuri ya mlima na maajabu ya kuwa na barafu kwenye maeneo ya tropiki wageni wanaotembelea mlima Kilimanjaro watafurahia kuona wanyama wengi walioko katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro“, alisema Dkt. Kijazi akitumia vizuri fursa hiyo kutangaza utalii katika mlima Kilimanjaro.

Aliongeza kwa kusema Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa taarifa mahususi kwaajili ya wakazi wa eneo la mlima Kilimanjaro kila inapotoa utabiri wa msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa ambapo wakazi wa maeneo hayo wanazitumia vyema taarifa za hali ya hewa kwaajili ya shughuli za maendeleo.

Aidha, aliainisha changamoto ya upungufu wa vituo vya hali ya hewa katika maeneo yanayozunguka mlima Kilimanjaro na kuelezea mikakati ya serikali kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa na vituo vya kutosha. Washiriki wa Mkutano huo waliipongeza Tanzania kupitia TMA kwa kutoa huduma bora za hali ya hewa katika eneo hilo la mlima Kilimanjaro.

Awali wakati wa ufunguzi, Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Taalas alizungumza kuhusiana na ripoti zinazotolewa na Taasisi inayofuatilia Mwenendo wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (IPCC) kuwa zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko kubwala joto katika maeneo mengi duniani hasa kwenye maeneo yenye milima mirefu hivyo kusababisha madhara mengi ikiwemo kuongezeka kwa kasi ya uyeyukaji wa barafu inayofunika vilele vya milima mirefu na kupelekea kuchangia upungufu wa maji na kuathiri shughuli mbali mbali za kijamii ikiwemo kilimo, ufugaji na upatikanaji wa umeme unaozalishwa kwa nguvu ya maporomoko ya maji kutoka milimani.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa makubaliano ya mambo muhimu ya kuzingatia katika kuhakikisha huduma bora za hali ya hewa zinatolewa katika maeneo ya milima mirefu duniani. Wadau wa maendeleo walihimizwa kutoa msaada kwa nchi zinazoendelea kuhakikisha huduma bora za hali ya hewa zinatolewa ili kulinda maisha ya watu na mali zao. Mkutano huo umejumuisha watalamu wa masuala ya hali ya hewa duniani ili kujadili namna bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika maeneo yenye milima yenye vilele virefu duniani. Tanzania ni moja ya maeneo yenye mlima mrefu duniani na wenye barafu ambao ni mlima Kilimanjaro.