Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

ISO 9001:2015 Certified in Aviation Meteorological Services

Habari

 • Utabiri wa Mvua kwa Wiki Mbili

  Imewekwa: 29th March, 2019

  Tarehe 29 Machi 2019

  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa hali ya hewa wa muda mfupi na muda wa kati kwa lengo la kuwapatia wananchi taarifa sahihi na za ziada kuhusu utabiri wa mvua iliokwishatolewa.

  Mwenendo wa mvua katika kipindi hicho hautarajiwi kubadili matarajio ya jumla ya mvua za Masika. Hivyo, msimu unatarajiwa kuwa mfupi na vipindi vya upungufu wa mvua za Masika vikijitokeza katika maeneo mengi.

  Mvua zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi yanayopata mvua za Masika baada ya athari ya upungufu wa mvua uliotokana na vimbunga vilivyojitokeza mfululizo katika bahari ya Hindi ikiwemo kimbunga Idai, Savannah na Joaninha katika mifumo ya hali ya hewa kuanza kupungua. Vipindi vya mvua vinatarajiwa kuongezeka katika baadhi ya maeneo katika wiki mbili zijazo za mwezi Aprili, 2019.

  Aidha, maeneo ya mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Kilimanjaro ambayo yalikumbwa na upungufu wa mvua kutokana na vimbunga hivyo, yanatarajiwa kuanza kupata mvua katika kipindi hiki cha mwishoni mwa mwezi Machi na wiki ya kwanza ya mwezi Aprili, 2019. Ongezeko la mvua linatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara hususan katika wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019 kwa siku chache.

  ANGALIZO: Vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo yafuatayo katika muda uliotajwa.

  i. Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kusini magharibi (mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Morogoro-Mahenge) na mikoa ya Lindi na Mtwara katika kipindi cha mwisho wa wiki kuanzia tarehe 30 Machi hadi 3 Aprili, 2019.

  ii. Mwanzoni mwa mwezi Aprili, 2019 vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza katika mkoa wa Morogoro na kusambaa katika maeneo machache ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

  HALI YA JOTO: Wimbi la joto lililojitokeza katika kipindi cha upungufu wa mvua katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki linatarajiwa kupungua kiasi katika kipindi cha uwepo wa mvua.

  USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

  Imetolewa na:

  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania


 • Weather by Region

  © 2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.