Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

ISO 9001:2015 Certified in Aviation Meteorological Services

Habari

 • TAARIFA YA VIPINDI VYA HALI YA JOTO KALI

  Imewekwa: 03rd December, 2018

  Kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia. Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine. Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba na mwezi Disemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Hali hii hushuhudiwa zaidi kunapokuwepo na upungufu wa mvua ambazo zingesaidia katika kupunguza hali ya joto katika kipindi husika.

  Wastani wa joto katika mwezi Novemba na Disemba ni nyuzi joto 31.5 kwa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba. Hata hivyo, mpaka kufika mwishoni mwa Novemba 2018 joto limeshafika nyuzi joto 34. Katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Morogoro, Dar es salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ambapo msimu wa mvua za Vuli unaendelea kukumbwa na mtawanyiko hafifu wa mvua hali ya fukuto inachangia katika hali ya joto japo vipimo vya nyuzi joto katika baadhi ya maeneo hayo ni vya wastani.

  Vipindi hivi vya joto kali vinatarajiwa kupungua kadiri mtawanyiko wa mvua za vuli utakavyoimarika katika mwezi Disemba 2018. Hata hivyo ikizingatiwa kuwa hali ya joto inatarajiwa kujirudia tena mnamo mwezi Februari 2019, wakati wa kipindi cha pili cha jua la utosi. Aidha, taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Hivyo tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki kila inapobidi.

 • Weather by Region

  © 2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.