Habari

Imewekwa: Sep, 07 2020

TMA YAWAZAWADIA WANAHABARI BORA WA HABARI ZA HALI YA HEWA.

TMA YAWAZAWADIA WANAHABARI BORA WA HABARI ZA HALI YA HEWA.

TMA, Makao Makuu-Dar es Salaam, Tarehe; 07/09/2020.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewazawadia wanahabari waliofanya vizuri katika kuandika habari za hali ya hewa kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Septemba 2019 hadi Septemba 2020. Tuzo hizo zilitolewa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani S. Nyenzi katika warsha ya wanahabari kuhusu mweleko wa msimu wa mvua za vuli 2020, ambaye aliwapongeza washindi wa tuzo hizo na kuwataka wanahabari wote kuendelea kuzipa taarifa za hali ya hewa kipaumbele zaidi na wasisite kuziwasilisha kwaajili ya ushindani.

“Shindano kama hili linaleta morali kwenu ninyi na hata kwa wanahabari wengine wasiokuwepo hapa, hivyo niwaahidi tu kuwa huu ni mwanzo na hizi tuzo zitaboreshwa zaidi hapo mbeleni na kuongeza ushindani, hivyo mjipange katika hilo”. Alizungumza Dkt. Nyenzi, Mgeni Rasmi wa tuzo hizo na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA.

“Hata kama TMA haijawaita kufanya kazi kwa mwaliko rasmi basi nyie mtumie weledi wenu kuzitafuta sehemu za kuzungumzia kwani ziko nyingi sana”. Aliongeza Dkt. Nyenzi.

Awali wakati akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa ili kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinaifikia jamii kwa wakati na usahihi, Mamlaka imekuwa ikitumia njia mbalimbali ikiwemo wanahabari ambao ni daraja muhimu katika kuwafikia wananchi wote.

“Katika kuonesha umuhimu wa tasnia hii, Tarehe 3 mwezi huu, Mamlaka ilikutana na wadau wa sekta zingine na baadhi yenu mlishiriki katika mkutano huo, lakini leo tumeamua kuwa na mkutano huu ambao ni mahususi kwa wanahabari peke yenu”. Alisema Dkt. Kijazi

Kwa upande wa mshindi wa kwanza wa tuzo hizo, Bi. Theopista Nsanzugwako kutoka gazeti la Habari Leo alitoa wito kwa wanahabari kuilisha jamii taarifa za hali ya hewa ili wananchi waweze kuzitumia katika kukabiliana na hali ya hewa husika, kwa vile hali ya hewa ni maisha.

Naye mshindi wa pili wa tuzo hizo, Bw. Jerome Risasi kutoka Clouds Media aliwahimiza wanahabari kufuatilia mara kwa mara taarifa za hali ya hewa zinazotolewa ili wananchi wapate taarifa za uhakika ikiwa ni pamoja na kujua athari za hali ilitolewa.

Lengo kuu la warsha hiyo lilikuwa kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2020 ili kupata uelewa wa pamoja na kurahisisha uwasilishwaji wake kwa jamii katika lugha inayoeleweka, pamoja na kuwapongeza wanahabari waliofanya vizuri kwa kipindi cha mwaka mmoja