Habari

Imewekwa: Mar, 19 2020

MHE. NDITIYE AAGIZA BARAZA LA TMA KUANDAA MIONGOZO NA MAFANIKO YENYE TIJA KWA SERIKALI.

MHE. NDITIYE AAGIZA BARAZA LA TMA KUANDAA MIONGOZO NA MAFANIKO YENYE TIJA KWA SERIKALI.

Dodoma, Tarehe: 16/03/2020;

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi na Mawasiliano) Mhe. Mhandisi. Atashasta Nditiye ameagiza wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuandaa miongozo na mafanikio yenye tija kwa Mamlaka na Serikali kupitia mijadala ya Baraza hilo.

Mhe. Mhandisi. Nditiye alitoa maagizo hayo wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) linalofanyika katika Ukumbi wa Takwimu, Dodoma, Tarehe 16 na 17 Machi 2020.

“Hakikisheni kwamba mnaweka vyema vipaumbele vyenu, na kutimiza mambo ya msingi kwanza ili kukabiliana na tatizo la ufinyu wa bajeti lililopo”. Alisema Mhe. Mhandisi. Nditiye

Aidha Mhe. Naibu Waziri aliitaka Mamlaka kuharakisha upatikanaji wa kanuni ili sheria ianze kufanya kazi kurahisisha ufanisi wa majukumu ya Mamlaka.

“Endeleeni kuboresha utabiri na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa wakati na kwa usahihi kwa jamii ya watanzania na wageni wanaotembelea nchini, kwa kusema hivi naamini michango yenu katika mkutano huu wa Baraza lenu la wafanyakazi, itatoa matokeo makubwa yatakayoendeleza sekta ya hali ya hewa nchini na pia kuliwezesha Taifa letu kusonga mbele kiuchumi na kimaendeleo”. Alisisitiza Mhe. Mhandsi. Nditiye.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi alimshukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kujumuika na wajumbe wa Baraza katika ufunguzi wa Baraza hilo na Wizara kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa iliyoonesha katika kuboresha muundo mpya wa Mamlaka unaolenga kuboresha maslahi ya wafanyakazi..

“Uwepo wako umetupa nguvu na ari mpya katika kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi hasa katika kipindi hiki ambacho TMA imekuwa Mamlaka kamili”.Alieleza Dkt. Kijazi

Aliendelea kwa kumueleza kuwa Baraza la mwaka huu ni kwa mujibu wa mkataba mpya kati ya Menejiment na TUGHE na linajumuisha wajumbe 98 kutoka vituo mbali mbali vya hali ya hewa hapa nchini ikijumuisha viongozi na wawakilishi wa wafanyakazi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Bi Jane Kikunya alimuomba Mhe. Naibu Waziri kusaidia katika kutatua changamoto ya ufinyu wa bajeti kwa kuongeza zaidi bajeti kwaajili ya kusaidia uboreshaji wa vifaa vya hali ya hewa

Mkutano huo wa Baraza ulianza na elimu ya namna ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Korona katika maeneo yao ya kazi na jamii kwa ujumla.