Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

ISO 9001:2015 Certified in Aviation Meteorological Services

Habari

 • MHE. PROF. KABUDI

  Imewekwa: 10th July, 2019

  ‘Nakuahidi kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano wote katika kutekeleza majukumu yako ndani ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)’. Alisema Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi.

  Katika mazungumzo hayo, Prof. Kabudi alisema Dkt. Kijazi amekuwa mfano kwa Tanzania na Afrika hususani kwa wanawake na kuahidi kutoa ushirikiano wenye lengo la kuhakikisha anafanikisha utekelezaji wa majukumu yake katika nafasi ya Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO na hivyo kuiwakilisha nchi vyema.

  Mhe. Prof Kabudi aliendelea kuelezea umuhimu wa kujiendeleza kielimu kwa watumishi wote wa Serikali ili kuweza kujijengea uwezo wa kupambana na watumishi au wagombea wengine kutoka mataifa mbalimbali hususan mataifa yaliyoendelea kwenye nafasi za juu za kidunia.

  Aidha, Mhe. Waziri alimtaka Mkurugenzi wa TMA kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa nchini kwa vile ni huduma muhimu sana kwa sekta zingine kama kilimo, uvuvi, mipango n.k, akitolea mfano wa kazi nzuri iliyofanyika ya kutoa tahadhari za mara kwa mara za mvua kubwa na kimbunga Kenneth ambazo zilisaidia Serikali kuchukua hatua stahiki

  Naye, Dkt. Kijazi aliishukuru Wizara kwa namna walivyofanikisha mchakato mzima wa uchaguzi hadi kupatikana kwa nafasi ya umakamu wa Tatu wa Rais wa WMO na aliahidi kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania vizuri, kwavile ameona jinsi diplomasia ya Tanzania inavyokubalika kimataifa.

  ‘Kwa vile moja ya jukumu langu kubwa nililopatiwa kusimamia ni eneo la kujengeana uwezo (capacity building), nitahakikisha mawazo ya nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania yanawasilishwa na kufanyiwa kazi kwa maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa na hivyo kuboresha huduma za hali ya hewa’. Alizungumza Dkt. Kijazi

  Aidha, aliishukuru Serikali, kupitia Wizira wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kumuani na kukubali kujitosa katika kinyanga’nyiro hicho. Aliiomba Serikali iendelee kufanya hivyo kwa wengine ili kukuza diplomasia ya Tanzania duniani.

 • Weather by Region

  © 2019 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa.